SWAUMU (FUNGA)

Swaum ni kujizuia na kula na kunywa na vitu vinginevyo katika muda maalum kwa nia ya kujikaribisha kwa mwenyezi mungu. Na ni moja wapo kati ya matawi ya dini yaliyo ya lazima.

SWAUMU NA MASHARTI YA KUWAJIBIKA KWAKE

Ni wajibu kwa kila muislaam kufunga mwezi wa ramadhani yanapo kamilika mashartyi yafuatayo:

1- Kubalee, si wajibu kwa mtu ambae hajafikia balee kuanzia mwanzoni mwa al fajiri ya mweziwa ramadhanikufynga, japo kuwa kauli ya ahwat inasema ya kuwa ni bora kuitimiza ikiwa amenuwia kufunga sunna na akabalee kati kati ya mchana.

2-3- Kuwa na akili timamu na asiwe amezimia, ikiwa atapatwa na wazimu  au kuzimia  kiasi kwamba nia  izingatiwayo kwenye swaumu ikampita  na akazindukana katikati ya mchana haita kuwa ni wajibu kwake kufunga siku hiyo, ndio ikiwa alitangulia kutia nia kabla ya kuzimia au kupatwa na wazimu kauli ya ahwat  ni kuwa itamlazimu kuikamilisha swaumu hiyo.

4- Asiwe na hedhi  wala nifasi, kwa hivyo basi si wajibu  kwa mwenye hedhi wala  mwenye nifasi kufunga  na haita swihi kwa watu hawa wawili funga hata kama hedhi au nifasi hiyo itakuwa ilichukua sehemu fulani ya siku (mchana).

5- Kuto kuwa na madhara katika funga,  kama akiwa na ugonjwa na ikiwa atafunga ataweza kudhurika  ima kwa kuzidisha ugonjwa huo au kuchelewa  kupona au kuzi kwa maumivu, na hayo  yote huangaliwa kiwango cha kawaida, na hakuna tofauti kati ya kuwa na yakini juu ya kupatikana madhara hayo au kuwa na dhanna juu ya kupatikana madhara  na kuwa na ihtimali ipelekeayo kukubali kuwepo kwa  khofu  itokanayo na vyanzo vya kiakili, katika mambo yote hayo si wajibu kufunga, na ikiwa atafahamu ya kuwa  hata pata madhara  kwenye nafsi yake lakini akaogopa madhara  kwenye heshima yake au mali yake pamoja na kutatizika katika kustahamili hali hizo haita kuwa ni wajibu kwake kufunga,  pia ikiwa atakuwa amesongwa na jambo la wajibu  lililo sawa  na hilo au lenye umuhimu  zaidi kama lau kama ataogopea  heshima ya mwenziwe au mali yake pamoja na kuwa ni wajibu  wake kuihifadhi.

6- Kuto kuwa msafiri,  lau kama atakuwa katika  safari ambayo ni juu yake kupunguza sala, haita kuwa wajibu kwake kufunga bali pia haiswihi funga yake, ndio safari ambayo ni wajibu kukamilisha sala saumu haita anguka yaani ni wajibu kufunga.

Mas’ala:  Sehemu ambazo msafiri ana hiari ya kupunguza au kukamilisha sala  itamlazimu sehemu hizo kula na swaumu haita swihi sehemu hizo.

Mas’ala:  Huzingatiwa katika kujuzu kula kwa msafiri kuwa awe amevuka mpaka wa mji wake, mpaka ambao huzingatiwa katika kupunguza sala na ufafanuzi wake umepita katika mas’ala ya  sala ya msafiri.

Mas’ala: ni wajibu –kwa kauli ya ahwat- kukamilisha funga kwa mtu ambae amesafiri  baada ya kupinduka kwa  jua na swaumu hiyo itatosheleza hakutakuwa na haja ya kuilipa, ama alie safiri kabla ya kupinduka jua  haiswihi kwake kufunga siku hiyo- japo kuwa atakuwa hakunuwia  safari kuanzia usiku kwa kauli ya ahwat- kwa hiyo inajuzu kwake kula  (kuto funga) baada ya kuuvuka mpaka wa mji wake na ni juu yake kuilipa swaimu hiyo.

Mas’ala: Ikiwa masafiri atarudi kwenye mji wake au kupita sehemu ambayo anakusudia kubakia hapo kwa muda wa siku kumi kuna sura zifuatazo:

 1- Arudi sehemu hiyo baada ya kupinduka kwa jua, katika hali kama hii si wajibu  kwake kufunga.

2- Awe amerudi kabla ya kupinduka kwa jua  na katika safari yake alikula, wakati huo si wajibu kwake kufunga pia.

3-Awe amerudi kabla ya kupinduka kwa jua na awe hakula katika safari yake, katika sura kama hii  ni wajibu kwake kunuwia funga na afunge kwa muda ulio bakia.

Mas’ala: ikiwa  msafiri atafunga  kwa kuto fahamu hukumu  na akafahamu hukumu hiyo baada ya kumalizika mchana,  funga yake itasihi na si wajibu kwake kuilipa na ikiwa atafahamu hukumu hiyo katikati ya mchana  saumu itabatilika na mtu alie sahau saumu yake haita swihi.

Mas’ala: Inajuzu kusafiri katika mwezi wa ramadhan hata kama si dharura, na nilazima kuto funga katika safari hiyo, ama katika mambo  mengine  maalum ya wajibu  kauli yenye nguvu inasema haijuzu kusafiri ikiwa jambo hilo ni wajibu kwa kuchukua malipo na mfano wake na vile vile siku ya tatu kati ya siku za itikafu, ama kauli iliyo dhahiri ni kuwa inajuzu kusafiri ikiwa wajibu huo ni kwa sababu ya nadhiri, ama yamini (kiapo) kukiunganisha na hukumu hiyo kuna ishkaali.

Mas’ala:  Funga ya wajibu haiswihi kwa msafiri ambae  katika safari yake  ni wajibu kupunguza sala- pamoja na kufahamu hukumu hiyo- isipokuwa katika sehemu tatu:

1- kufunga siku tatu  nazo ni siku ambazo  ni baadhi ya siku kumi ambazo zinakuwa badala ya hadyu (mnyama katika hajji ya tamattui kwa yule ambae atashindwa kuitekeleza.

2-Kufunga siku kumi na nane ambazo ni badala ya mnyama ikiwa  ni kafara kwa mwenye kutoka arafa kabla ya kuzama jua.

3- Kufunga swaumu ya sunna ambayo imetiliwa nadhiri  kuifungakatika  safari  sehemu nyingine sawa iwe safari au nyumbani, kama ambavyo haiswihi kufunga saumu ya wajibu  safarini tofauti na sehemu zilizo tajwa, vile vile haisihi kufunga saumu ya sunna isipokuwa siku tatu kwa ajili ya hajja  katika mji  mtukufu wa madina na kauli ya ahwat ni kuwa iwe siku ya juma tano, al khamisi, na ijumaa

Mas’ala: Huzingatiwa katika kusihi kwa funga ya sunna ya kuwa mtu asiwe na dhima ya kulipa funga ya mwezi wa Ramadhani, na hakuna madhara ikiwa atakuwa na funga ya wajibu kwa kuchukua malipo au ya kulipa kadhaa au ya kafara na mfano wa hizo, ikiwa anafunga hizo itajuzu kwake kufunga saumu ya sunna katika sehemu zote hizo kwa kauli ya adh’har, kama ambavyo inaswihi kwake funga ya sunna  ambayo inaswihi kuifungia safarini hata kama atakuwas na kadhaa ya mwezi wa ramadhani kutokana na kauli ya ahwat na inajuzu kwake kuchukua ujira kwa ajili ya kufunga swaumu ya wajibu kwa ajili ya mtu mwingine au kumfungia kwa kujitolea  kabla  ya kulipa swaumu zake za mwezi wa Ramadhani.

Mas’ala:  Mzee wa kiume na kike pindi ikiwawia vigumu kufunga inajuzu kwao kula na badala yake watatoa  kibaba kimoja  cha chakula kila siku ikiwa ni kafara ya siku hiyo, na si wajibu kwako kuilipa siku hiyo, na ikiwa watashindwa kufunga basi funga itaanguka kwao na vile vile wakati huo kafara itaanguka, na hukumu hii hutumika kwa mwenye kiu ( yaani mwenye ugonjwa wa kiu) pia  ikiwa funga itamtatiza atatoa kila siku kibaba kimoja cha chakula na ikiwa hakuweza kutoa kibaba hicho pia uwezekano wa kafara kuporomoka upo.

Mas’ala:  mama mja mzito ambae siku zake zimekaribia ikiwa ataogopa kupatwa na madhara  yeye mwenyewe au mwanae itajuzu kula- bali huenda ikiwa wajibu kama ikiwa funga  itamlazimu kupata madhara yaliyo haramishwa kwa mmoja kati ya watu hao wawili- na atatoa kafara kila siku ya kibaba kimoja cha chakula na ni wajibu kwake kuilipa funga hiyo.

Mnyonyeshaji  mwenye maziwa kidogo ikiwa ataogopa yeye mwenyewe kupatwa na madhara au mwanae anae nyonya itajuzu kwake kula- bali pengine huenda ikawa wajibu kama  tulivyo sema katika mas’ala yaliyo tangulia- na ni juu yake kuzilipa siku hizo na kutoa kafara kwa kila siku kibaba kimoja cha chakula, na hakuna tofauti kati ya mnyonyeshaji sawa awe mama au mtu alie chukua ujira kwa kazi hiyo au mwenye kujitolea kufanya kazi hiyo, na kauli ya ahwat inasema ya kuwa ni lazima hukumu hii itumike pale tu ikiwa njia pekee ya kunyonyesha ni hii na hakuna njia nyingine ya kumnyonyesha mototo isipo kuwa hii  hata kama ni kutumia njia nyingine ikiwa hakuna kizuwizi, ama ikiwa kuna uwezekano huo haitajuzu kwake kula.

Mas’ala: Kibaba cha chakula ni sawa na kilo tatu takriban,na ni bora zaidi kiwe ni kibaba cha ngano au unga wangano na kauli ya adh;har ni kuwa inafaa aina yoyote ya chakula hata kama ni mkate.

 KUTHIBITI KWA MWEZI WA RAMADHANI

Mas’ala: 1-Huzingatiwa katika  kuthibiti kwa mwezi  wa ramadhani na kuwajibika kufunga  mwezi wa Ramadhani  njia hizi zifuatazo:

1- Mukallaf  auone mwezi yeye mwenyewe.  2- Apate yakini au matumaini kutokana na kuenea kwa habari za kuonekana  kwa mwezi huo au habari zingine zithibitishazo suala hilo katika nchi yake au sehemu yenye hukumu kama hiyo. 

3- Kupita siku thalathini  za mwezi wa shaaban.  4-Kutoa ushahidi  wanaume wawili waadilifu ya kuwa wameuona ( na hapo nyuma tumekwisha elezee maana ya uadilifu ) na huzingatiwa kuwa kinacho tolewa ushahidi kiwe ni kimoja, lau mmoja wao atadai ya kuwa ameuona mwezi katika upande fulani, na mwingine akadai ya kuwa ameuona upande mwingine, kwa ushahidi huo mwezi hautathibiti, kama ambavyo huzingatiwa kutokuwepo mpingaji  wa ushahidi huo- hata kama kwa kuonyesha kitendo chenye hukumu kama hiyo ya kupinga- kama ikiwa  kundi la watu fulani wa nchi hiyo  watatoa habari za kuonekana mwezi na wakadai kuwa wameuona mwezi na miongoni mwao kukiwemo waadifu wawili, au wakatoa habari za kuonekana mwezi  kundi fulani lakini hawakudai ya kuwa wameuona mwezi isipokuwa waadilifu wawili  na wengine hawakuuona na miongoni mwao kukiwa na waadilifu wawili  ambao ndio wanao wawakilisha katika kufahamu sehemu pekee iliyo onekana mwezi kwa kuangalia pamoja na anga kuwa safi na kutokuwepo kinacho tarajiwa kuwa ni kizuwizi cha kuuona mwezi, katika hali kama hii ushahidi wa watu wawili waadiofu hauna iitibari yoyote, isipo kuwa ikipatikana yakiini na matumaini kutokana na ushahidi wao.

Mas’ala:  Mwezi hauthibiti kwa hukumu ya hakimu wala kwa kuwa kwake na duara iwe dalili  ya kuwa ulikuwa ni  wa usiku  ulio pita, ndio ikiwa hukumu yake itampatia matumaini na kumthibitishia  ya kuwa mwezu umeonekana katika nchi hiyo au sehemu ambayo hukumu  yake ni  sawa na nchi yake na hakutegemea kauli ya mtabiri au mnajimu au mfano wa hao.

Mas’ala: Ikiwa mukallaf atakula kisha ikabainika kuthibiti kwa hilali kupitia moja wapo kati ya njia  zilizo tajwa  itawajibika kuilipa funga hiyo, na ikiwa itathibiti huku imebakia  sehemu ya mchana  itawajibika kufunga sehemu hiyo iliyo bakia kutokana na kauli ya ahwat.

Mas’ala: Ina tosha kuthibiti mwezi katika nchi fulani hata kama si  katika nchi ya mfungaji ikiwa machweo ya nchi hizo ni mamoja, kwa maana kuwa  mwezi ukionekana katika nchi moja ni lazima uonekana katika nchi ya pili kama hakuna kizuwizi kama  mawingu au mlima au mfano wa hayo, kwa hivyo ikiwa mwezi utaonekana  katika nchi za mashariki ni lazima uwe umethibiti kwenye nchi za magharibi pia  lakini kwa kuzingatia kuwa kusiwe na umbali zaidi  katika machweo,   ama ikiwa utathibiti katika nchi za magharibi si lazima kuthibiti katika  mashariki isipokuwa ikiwa zinakaribiana katika machweo  katika misitari ya(Al aradh)na hapakuwa na urefu  wa kijografia  wenye umbali wa kiasi cha kilometa (880).

Mas’ala: Ni lazima katika kuthibiti kwa mwezi wa shawwal kuthibiti  mojawapo kati mambo yaliyo tangulia lau kamahalikuthibiti jambo lolote kati ya hayo  haitajuzu kula.

Mas’ala: Ikiwa mtu atafunga siku yashaka katika mwezi wa shawwal, kisha mwezi ukathibiti  katikati ya mchana itakuwa ni wajibu kwake kula.

Mas’ala: Haijuzu kufunga siku ya shaka ya mwezi wa ramadhani  kwa kukusudia kuwa ni katika mwezi wa Ramadhani, ndio inajuzu kufunga  kwa lengo kuwa ikiwa ni katika mwezi wa shaaban  funga yake itakuwa ni funga ya sunna au kadhaa na ikiwa ni katika mwezi wa ramadhani  itakuwa ni funga ya wajibu na funga yake itakuwa sahihi.

Mas’ala: Ikiwa  itatokea kuwa mtu anaishi sehemu ambayo  mchana wake ni miezi sita na usiku wake ni miezi sita au mchana wake ni miezi mitatu na usiku wake ni miezi tisa  au mfano wa hivyo  kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa ni juu yake kuangalia na kuchunga  sehemu zilizo karibu nae  ambazo zinapata usiku na mchana katika muda wa masaa ishirini na nne na atasali sala tano kulingana na wakati wa sehemu hizo kwa nia ya kujikurubisha kwa Allah  moja kwa moja, ama katika funga  itawajibika kwake kuhamia katika nchi ambayo anaweza kufunga,  ima iwe ni katika mwezi wa ramadhani au baada ya ramadhan, na ikiwa hakuweza kufanya hivyo  ni juu yake kutoa fidia, na ikiwa atakuwa katika nchi amabyo ina usiku na mchana  katika muda wa masaa ishirini na nne- hata kama mchana wake ni masaa ishirini na tatu  na usiku wake ni saa moja au kinyume chake- sala yake itasaliwa kulingana  na wakati wake maalum katika nchi hiyo,  ama funga ya mwezi wa ramadhan  ni wajibu kwake  kuitekeleza katika wakati wake  hata kama utapungua, maadam jua lina chomoza na kuzama na ita anguka  ikiwa hakuweza  na ikiwa ataweza kuilipa  ni wajibu kuilipa la sivyo ni juu yake kutoa fidia.

NIA YA FUNGA  (SWAUMU)

Ni wajibu kwa kila mukallaf kukusudia  kujizuwia na mambo yanayo funguza  ambayo yanajulikana, kuanzia alfajiri inapo chomoza  hadi linapo zama jua  kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah mtukufu,  na kauli ya adh’har ni kuwa inajuzu  kutosheka  na makusudio ya  kufunga mwezi mzima toka mwanzo wake,  kwa hiyo haizingatiwi kukusudia katika kila usiku au kutia nia kila siku au wakati wa kuchomoza alfajiri japo kuwa huzingatiwa kuwepo kwa nia hiyo hata kama ni kwa kujua kuwa ni kitu gani akifanyacho.

Mas’ala: Kama ambavyo huzingatiwa nia katika mwezi wa ramadhani vile vile huzingatiwa katika  funga zingine za wajibu, kama funga ya kafara, nadhiri , kadhaa, na funga kwa niaba ya mtu mwingine, lau kama mukallaf atakuwa na jukumu la kutekeleza funga kadhaa za wajibu ni juu yake kuziainisha  kwa kuongezea katika makusudio yake  (Nia), ndio hakuna haja ya  kuainisha katika mwezi wa ramadhani kwa sababu funga katika mwezi wa ramadhani  inajitambulisha yanyawe.

Mas’ala: Katika nia ya funga inatosha kunuwia kuwa ninajizuwia na vitu ninavyo funguza  kwa sura ya ujumla na hakuna haja ya kuviainisha kila kimoja.

Mas’ala:  Ikiwa  mtu hakutia nia siku moja wapo katika mwezi wa ramadhani  kwa kusahau  ya kuwa yuko ndani ya mwezi wa ramadhani  kwa mfano na hakula kitu chochote,  ikiwa atakumbuka baada ya kupinduka kwa jua ni wajibu  wake kutokana na kauli ya ahwat ya wajibu kufunga sehemu ya chana iliyo bakia kwa makusudio ya kujikaribisha kwa Allah na baadae atailipa,na ikiwa atakumbuka kabla ya kupinduka kwa jua   atanuwia funga  na funga hiyo itatosheleza  kutokana na kauli ya adh’har japo kuwa kauli ya ahwat inasema kuwa inabidi kuilipa baada ya hapo, vile vile katika funga zingine za wajibu ambazo ni maalum, ama funga za wajibu ambazo si zenye kuainishwa  wakati na nia yake huendelea hadi jua linapo pinduka, ama funga ya sunna  wakati wake wa kutia nia hurefuka hadi kufikia magharibi kwa maana kuwa mukallaf ikiwa hakula  inajuzu kwake  kutia nia ya sunna  na kufunga sehemu ya mchana iliyo bakia  hata kama itakuwa imebakia sehemu ndogo ya mchana na huhesabiwa kuwa amefunga siku hiyo.

Mas’ala: Lau kama mtu atanuwia funga kisha  akanuwia kula au akakusudia kula katika wakati ambao haijuzu katika wakati huo kuchelewesha nia kwa makusudi kisha akabadilisha tena nia  kwa kauli ya ahwat nia hiyo haitatosheleza.

Mas’ala: Ikiwa  mukallaf atakusudia usiku kufunga siku ya kesho, kisha akalala na hakuweza kuamka  mchana kutwa  funga yake ni sahihi,  ama ikiwa atalala hadi kupinduka kwa jua  na hakutia nia kabla,  kauli ya ahwat ni kuwa atatimiza siku ile kisha atailipa kadhaa.

YANAYO FUNGUZA SWAUMU

Mambo yafunguzayo swaumu ni haya yafuatayo:  1-2  (Kukusudia kula na kunywa)

Na hakuna  tofauti  katika vitu viliwavyo na vinywewavyo sawa viwe ni vile vijulikanavyo au vinginevyo, wala  hakuna tofauti  kati ya chakula hicho kiwe  kingi au kichache, kama ambavyo  hakuna tofauti  katika kula na kunywa iwe ni kwa njia ya kawaida au  njia nyingineyo,  lau kama mtu atakunywa maji kwa kupitia puani funga yake inabatilika, na funga itabatilika kwa kumeza chembe chembe za chakula zilizo bakia  katika kinywa au kwenye meno kwa hiyari.

Mas’ala: Funga haibatiliki kwa kula au kunywa kusiko kwa makusudi,  kama akisahau na akala au kunywa, vile vile haibatiliki ikiwa atavitapitiliza  kwenye koo lake  bila hiyari au mfano wa hayo.

Mas’ala: Haibatiliki funga kwa kujiwekea dawa kupitia njia ya  sindano katika viungo fulani au kwenye mishipa, hata kama itakuwa inafanya kazi ya chakula  kama vyakula vilivyo zoweleka katika zama zetu kama ambavyo haibatiliki  kwa kudondoshea matone masikioni au machoni  hata kama itadhihiri athari zake kama rangi au ladha kooni.

Mas’ala:  Ina juzu kwa mwenye funga kumeza mate  kwa hiyari yake ikiwa bado hayajatoka  mdomoni mwake bali inajuzu kwake kuyakusanya mdomoni kisha kuyameza.

Mas’ala: Hakuna shaka kwa mwenye kufunga kumeza makoozi  yatokayokifuani au yatokayo kichwani  ikiwa hayaja fika mdomoni ama yakifika mdomoni  kauli ya ahwat ni kuto yameza.

Mas’ala: Ina juzu kwa mwenye kufunga kupiga mswaki,  lakini  ikiwa mswaki utatoka mdomoni haijuzu kuurudisha  mdomoni  hali ya kuwa una umajimaji isipokuwa ikiwa atayatema  mate yaliyomo mdomoni mwake baada ya kuurudisha,  ndio ikiwa  maji maji yatakuwa machache kuliko mate yaliyomo kinywani mwake  kiasi kwamba maji maji yale hayakuonekana   yaliyo toka nje, hapo inajuzu kuyameza.

Mas’ala: Ina juzu kwa mwenye kutaka kufunga kuacha kuchokonoa meno  baadaya kula ikiwa atafahamu ya kuwa hakuna vyakula vilivyo ingia  na kubakia kwenye meno  hadi katikati ya mchana, laa sivyo itakuwa ni wajibu kuchokonoa meno hayo.

Mas’ala; Hakuna shaka kwa mwenye funga kumtafunia mtoto chakula  au mnyama  na inajuzu kuonja mchuzi  na mfano wa hayo  kati ya vitu ambavyo havi vuki na kufika  kooni, lau  kama itatokea chembe za chakula kuvuka  na kufika kooni bila ya kukusudia  wala  kujua ya kuwa itavuka  kwa nguvu au kwa kusahau funga yake haitabatilika.

Mas’ala; Inajuzu kwa mwenye kufunga kusukutua maji kinywani  kwa malengo ya kutawadha au  kwa ajili ya malengo mengine kwa sharti kuwa asimeze chembe yoyote ya maji kwa makusudi, na ni sunna baada ya kusukutua ateme mate mara tatu.

Mas’ala: Ikiwa mwenye kufunga ataingiza maji kinywani mwake kwa ajili ya kusukutua  au kwa sababu nyingine na maji yakapitiliza hadi kooni mwake  bila hiyari yake  ikiwa aliyaweka akiwa na kiu kwa ajili ya kupoza  koo au kinywa ni wajibu kwake kuilipa, ama ikiwa alifanya hivyo tofauti na hivyo  kati ya sehemu zinazo bidi kuingiza maji kinywani au puani na kuvuka hadi kooni  bila ya hiyari yake  kauli ya adh’har ni kuwa si wajibu kulipa  japo kuwa kauli ya ahwati ni kuwa  hata lipa ikiwa alifanya  hivyo katika hali  ya kutawadha kwa ajili ya sala ya sunna bali kwa kitendo chochote ikiwa  haikuwa ni kwa ajili ya sala ya sunna bali hata kama haikuwa ni kwa ajili ya  sala ya faradhi.

Mas’ala: (Kitu cha tatu kati ya vitu vinavyo funguza: kutokana na kauli ahwat ni kuzowea kumsingizia mwenyezi mungu  na mtume wake uongo au yeyote kati ya maimam watakasifu juu yao amani)  na huunganishwa na fatimas asswiddika  alie twaharika  na mitume wengine na mawasii wao  amani iwe juu yao.

Mas’ala: Ikiwa mwenye kufunga ataitakidi ya kuwa habari alizo zitoa kuhusiana na mwwenyezi mungu  au mmoja wapo kati ya maasumiina  ya kuwa ni za kweli  kisha ikambainikia kuwa ni uongo funga yake haita batilika, ndio ikiwa atatoa habari kuhusiana na mwenyezi mungu au kuhusu mtume wake  bila kujitegemeza kwenye hojja ya kisheria  pamoja na kuwa kulikuwa na ihtimali ya kuwa habari hizo ni uongo  na kweli habari hizo zikawa ni uiongo hukumu yake ni sawa na hukumu ya kukusudia kusema uongo.

Hakuna  shaka kuwa inafaa kusoma qur ani kwa kukosea ikiwa msomaji hakuwa katika hali ya kutoa masimulizi yaliyo teremshwa katika qur ani, na funga yake haitabatilika kwa kufanya hivyo.

Mas’ala: Jambo la nne kati ya vitu ninavyo funguza: - kwa kauli iliyo mashuhuri- (kupiga mbizi kwenye maji kwa makusudi) lakini kwa kauli iliyo adh’har ni kuwa haidhuru katika kuswihi kwa funga  bali ni makruhu karaha iliyo kubwa, na hakuna tofauti katika swala hilo kati ya kuzamisha kiwili wili chote au kichwa pekee, na hakuna shaka yoyote kwa mwenye kufunga kusimama chini ya mvua huku ikinyesha na mfano wa hilo hata kama maji yataufunika mwili wake wote.

Mas’ala: Kuli ya ahwat inasema kuwa ni juu ya mwenye kufunga  katika mwezi wa ramadhani na katika funga zingine kuto piga mbizi au kuzamisha kicha katika maji  japo kuwa kauli ya adh’har inasema kuwa inajuzu kufanya hivyo.    

Mas’ala: Jambo latano kati ya vitu vinavyo funguza:( Kukusudia kufanya tendo la kijinsia  ambalo hupelekea kupata janaba) na funga haitabatilika kwa kufanya tendo hilo ikiwa si kwa makusudi.

Mas’ala: Jambo la  sita kati ya vitu vinavyo funguza:(  kupiga kunyeto kwa kuchezea kiungo cha kiume au kuibusu (kuinyonya) au kuichezea kwa kuigusa  na mengineyo yasiyo hayo) bali akifanya chochote kati ya hayo, na alifanya hivyo bila kuwa na uhakika ya kuwa manii hayatatoka, kwa ghafla yakatoka  funga yake itabatilika kutokana na kauli ya adh’har.

Mas’ala: Ikiwa mtu atajiotea katika mwezi wa ramadhani  inajuzukwake kufanya istibraa kwa kukojoa  na awe na yakini ya kuwa chembe chembe zilizo bakia za manii zimetoka katika mirija ipitayo manii bila ya kutofautisha ya kuwa istibra hiyo iwe kabla ya kuoga au baada ya kuoga japo kuwa kauli ya ahwat inasema kuwa ni bora kuacha  katika sehemu ya pili (yaani baada ya kuoga).

Mas’ala: Jambo la saba  kati vitu vinavyo  funguza :( Kukusudia kubakia na janaba hadi kuchomoza kwa alfajiri) na hukumu hii inahusika tu na funga ya mwezi wa ramadhani na kadhaa yake, ama katika funga zingine kati ya mgawanyiko wa funga kauli ya dhahiri ni kuwa funga haita batilika katika hali kama hiyo japo kuwa kauli ya ahwat ni kuwa ni bora  kuiacha katika funga zingine za wajibu, kama ambavyo kauli ya ahwatul awlaa ni  kuto ilipa funga ya mweziwa ramadhani katika siku ambazo  atabakia akiwa na janaba hadi kuchomoza kwa alfajiri bila ya kukusudia.

Mas’ala: Kubakia na hadathi ya hedhi au Nifasi pamoja na kuwepo uwezekano wa kuoga au kutayammam  hukumu yake ni sawa na tuliyo seme kwa mwenye kukusudia kubakia kwernye janaba  bali hata kwa mwenye kulipa kadhaa pia kutokana na kauli ya  ahwat tofauti na funga zungine.

Mas’ala: Mwenye kupatwa  na janaba katika usiku wa mwezi wa ramadhani, kisha akalala bila ya kukusudia kuoga- ikiwa alinuwia kuto oga,  bali vile vile ikiwa atakuwa ni  mwenye wasi wasi kuhusiana na ghusli hiyo- na akaamka baada ya alfajiri hukumu yake ni sawa na hukumu ya alie kusudia kubakia kwenye janaba, ama ikiwa alikusudia kuoga janaba na akawa na yakini ya kuwa ataamka- kutokana na kuzowea au jambo lingine- ikatokea kuwa hakuweza kuamka isipokuwa baada ya alfajiri  hakuna jukumu lolote juu yake na funga yake ni sahahi, ndio  ikiwa ataamka kisha akalala  na hakuweza kuamka  hadi ikachomoza alfajiri  ni wajibu wake kulipa kadhaa baada ya kumalizika, vilevile hali ni hiyo hiyo ikiwa atalala mara tatu isipo kuwa ni kwamba kutokana na  kauli ya ahwatul awlaa ni kuwa atatoa kafara katika siku hiyo pia.

Mas’ala: Ikiwa atapatwa na janaba katika usiku wa   mwezi wa ramadhani  na akalala hali ya kuwa amenuwia au amekusudia kuoga  lakini hakuwa na yakini ya kuwa ataweza kuamka,  kauli ya ahwat ni kuwa ni lazima kuoga kabla ya kulala, na ikiwa atalala na hakuweza kuamka kauli ya ahwat ni kuwa atailipa funga hiyo hata katika ulalaji wake wa mwanzo, bali kauli ya ahwat ni kuwa atatoa kafara pia na hasa katika ulalaji wake wa tatu.

Mas’ala: Ikiwa mukallafu ataelewa ya kuwa anayo janaba lakini akasahau kuoga janaba hiyo hadi kuchomoza kwa alfajiri ya mchana wa mwezi wa ramadhani itakuwa ni juu yake kuilipa funga hiyo lakini ni wajibu wake kufunga siku hiyo  kwa makusudia ya kutekeleza  wajibu ulioko kwenye dhima yake kutokana na kauli ya ahwat, na kauli yenye nguvu zaidi ni kuwa hukumu hii haitaunganishwa na funga isiyo kuwa ya mwezi wa ramadhani katika suala hilo hata katika kadhaa yake kama ilivyo tangulia, na kikiwa hakufahamu ya kuwa alikuwa na janaba au ali fahamu ya kuwa ana janaba  na akasahau wajibu wa kufunga  siku ya kesho hadi ikachomoza alfajiri funga yake itakuwa sahihi na hakuna lolote juu yake.

Mas’ala: Ikiwa mwenye janaba hakuweza kuoga usiku, ni wajibu wake kutayammam kabla ya kuchomoza alfajiri  badala ya kuoga na ikiwa ataacha  kutayammam  funga yake itabatilika kutokana na  kauli ya adh’har, na si wajibu kwake kubakia akiwa macho baada yake hadi kuchomoza kwa alfajiri japo kuwa  kufanya hivyo ni ahwat, na ikiwa alikuwa na uwezo wa kuoga na hakufanya hivyo hadi muda ukawa finyu na hakutayammam, funga yake itabatilika.

Mas’ala: Hukumu ya mwanamke katika hali ya istihadha ndogo ni sawa na hukumu ya mwenye twahara, ama katika istihadha nyingi kauli iliyo mashuhuri ni kuwa  huzingatiwa  kuoga  ghusli za   mchana  na usiku ulio pita katika kuswihi kwa funga yake, lakini kauli ya kuto zingatia uogaji huo haiko mabali japo kuwa kufanya hivyo ni ahwat, bali kauli ya ahwati ni kuwa  inambidi kuoga kwa ajili ya salaya asubuhi kabla ya kuchomoza alfajiri kisha  atarudia baada yake, ama katika hali ya istihadha  mutawassit kauli iliyo adh’har ni kuwa hataizingatia ghusli hiyo katika kusihi kwa  funga yake, japo kuwa kauli ya ahwat ni kuwa itambidi kuoga pia.

Mas’ala: jambo la nane kati ya vitu ninavyo funguza: (Kukusudia kuingiza vumbi au  moshi mzito kooni kwa kauli ya ahwat)  na hakuna shaka ikiwa vumbi hilo au moshi huo si mzito, vile vile moshi au vumbi ambalo ni vigumu kujikinga nalo kwa kawaida kama vumbi lililo timuliwa na hewa au upepo.

Mas’ala: jambo la tisa kati ya vitu vinavyo funguza:( Kujitapisha kwa makusudi) na inajuzu kwa mwenye kufunga  kupiga mbwewe  hata kama atakuwa na ihtimali ya kutoka kwa chembe za chakula au kinywaji  kwa pamoja na kauli ya ahwat ni kuwa ni bora kuto fanya hivyo ikiwa atakuwa na yakini ya kutoka kwa  chakula.

Mas’ala: Ikiwa atapiga mbori na kutoka chakula  hadi kooni au kikatoka kwa sababu nyingine ile bila ya kukusudia  haita juzu kukimeza kwa mara ya pili, na ikiwa atakimeza hukumu yake ni sawa na hukumu ya kula na kunywa kwa kauli ya ahwat.

Mas’ala: Jambo la kumi kati ya vitu vinavyo funguza:( Kukusudia  kuingiza maji  mwilini kupitia mishipa au njia nyingioneyo au chochote chenye maji maji) hakuna shaka ikiwa kitu hicho hakina umaji maji.

Mas’ala: Nyongeza: - Mambo yafunguzayo yaliyo tangulia- tofauti na kula na kunywa na kufanya tendo la kijinsia- hubatilisha funga ikiwa  yatafanywa na mwenye kufahamu ya kuwa ni vitu vinavyo funguza au jahili mukaswir ( yaani asie fahamu na kuto fahamu huko hakutokani na uzembe wake), vile vile asie kuwa mukassir ikiwa alikuwa ni mwenye kutaradadi, na hilo haliifanyi funga kubatilika ikiwa atafanya bila kukusudia  katika kuto kufunguza kwake kwa hoja ya kisheria au kutokana na ujahili murakkab  ikiwa imetokana na uzembe wake mwenyewe.

HUKUMU YA VITU  VINAVYO FUNGUZA

Ni wajibu kutoa kafara kwa kila mwenye kuacha kufunga mwezi wa ramadhani  kwa kula au kunywa au kufanya tendo la kijinsia au kupiga kunyeto  au kubakia na janaba kwa makusudi  na kwa hiyari bila ya kulazimishwa  wala kukarahishwa, na inathibiti kafara kwa  kumkomboa mtumwa au kuwalisha masiki sitini  au kufunga miezi miwili mfululizo, yaani kufunga mwezi wa kwanza kamili  na katika mwezi wa pili akafunga japo kuwa siku moja, na siku zilizo bakia akazifunga siku yoyote ile, na hii ikiwa futari  aliyo itumia ni ya halali ama ikiwa ni ya haram, kauli ya ahwatul awlaa ni kuwa atatekeleza mambo yote yaliyo tajwa na kama hakuweza kuyatekeleza yote atatekeleza tu yale awezayo kuyatekeleza.

Mas’ala: Ikiwa mwenye kufunga atamlazimisha mkewe  kufanya tendo la ndoa  katika mchana wa mwezi wa ramadhani nae akiwa amefunga  kafara zitaongezeka juu yake kutokana na  kauli ya ahwat na ata adhirishwa hadharani kutokana na hukumu ya hakimu wa kisheria, na ikiwa hakumlazimisha na akafanya kitendo hicho kwa ridhaa yake mwamamke  ni juu ya kila mmoja kutoa kafara moja na wata adhiriwa  kulingana na aonavyo hakimu wa kisheria pia.

Mas’ala: Mtu yeyote atakae kula katika siku ya funga ya mwezi wa ramadhani  na funga yake kubatilika ni wajibu kwake kujizuwia kula sehemu iliyo bakia ya siku hiyo moja kwa moja kwa kauli ya ahwat, bali kauli ya ahwat ni kuwa kujizuwia huko kuwe ni kwa makusudio ya kujikaribisha kwa Allah  katika kuingiza moshi au vumbi zito kooni na katika kumzulia mwenyezi mungu na mtume, na kafara haiwi wajibu isipo kuwa kwa  ulaji wa mara ya kwanza  na haikaririki kwa kula mara kadhaa hata katika kufanya tendo la kijinsia na kupiga kunyeto hakika kauli ya adh’har ni kuwa kafara haikaririki kwa kukaririka kitendo hicho japo kuwa  ni ahwat kufanya hivyo.

Mas’ala: Mwenye kula katika mwezi waramadhani kwa makusudi kisha akasafiri, wajibu wa kutoa kafara hauta anguka hata kama safari yake itakuwa kabla ya kupinduka kwa jua.

Mas’ala: Wajibu wa kutoa kafara unahusika na mwenye kufahamu hukumu,  hakuna kafara kwa mtu asie fahamu hukumu, kutofahamu huko kutokane na uzembe wake au laa- na asiwe mwenye kutaradudi-kwa kauli ya adh’har, lau kama atatumia kitu kinacho funguza kwa kuitakidi ya kuwa  hakibatilishi funga  haita kuwa ni wajibu kwake kutoa kafara sawa awe ameitakidi kuwa ni haramu katika nafsi yake au laa kwa kauli iliyo aqwaa,  lau kama atapiga kunyeto kwa makusudi akifahamu uharamu wa kufanya hivyo akiitakidi- hata kama ni kwa  uzembe wake mwenyewe- kuto batilika kwa funga  kwa kufanya hivyo hana jukumu la kutoa kafara, ndio haizingatiwi  katika wajibu wa kutoa kafara kufahamu  kuwa ni wajibu na haijuzu kujionyesha kuwa  hukufunga katika mwezi wa ramadhani ikiwa kufanya hivyo itahesabiwa kuwa ni  kuvunja  na kuto uheshimu mwezi wa ramadhani isipo kuwa kwa mwenye udhuru, na ambae udhuru wake huonekana katika mandhari yake kama mtu  kikongwe au mgonjwa ambae zinaonekana kwake dalili za ugonjwa na kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa ni bora kutompatia chakula  mwenye matatizo kwa makusudi  na sio kwa udhuri.

SEHEMU  AMBAZONI WAJIBU KULIPA TU

Mas’ala:Mwenye kula katika mwezi wa ramadhani kutokana na udhuru au ugonjwa  na mfano wa hayo ni wajibu wake kulipa  siku hiyo katika miezi mingineyo na katika siku zingine za mwaka huo isipo kuwa siku mbili za idi (iidul fitri  na idul adh’haa) haijuzu kufunga  kadhaa katika siku mbili hizi au funga nyingine yoyote isiyo ya kadhaa kati ya funga  zingine kama funga za sunna.

Mas’ala: Mwenye kulazimishwa kula au kunywa  au kufanya tendoa la kijinsia katika mwezi wa ramadhani  au kutokana na takiyya ikamlazimu kufanya tendo hilo  au alilazimika kufanya hivyo au alilazimika kutapika au kujichoma dawa, inajuzu kwake kula  kwa kiwango au kisi cha dharura ilivyo,  lakini funga yake inabatilika na niwajibu kwake kuilipa  bali kauli ya ahwat ni kuwa ni lazima kuilipa  ikiwa atalazimishwa kula  tofauti na sehemu tatu zilizo tangulia vilevile.

Mas’ala: Katika sehemu zilizo tangulia zimetajwa sehemu  zinazowajibika kulipa tu na zingine ni kamazifuatazo: 

1- Pindi nia ikiingiwa na kasoro katika mwezi wa ramadhani  lakinihakufanya  jambo lolote linalo funguza  kati ya mambo yaliyo tajwa.

2-  Pindiakifanya jambo moja wapo kati ya mambo yafunguzayo bila ya kufanya uchunguzi kama  alfajiri imechomoza,  na wakati anakula ikadhihiri ya kuwa alfajiri imekwisha chomoza, wakati huo ni wajibu wake kutokula kwa malengo ya kujikaribisha kwa Allah kwa kauli ya ahwat na baadae atailipa, ama ikiwa atafanya uchunguzi na  hakuona kuwa alfajiri imechomoza  na akala  kisha ikabainika ya kuwa imekwisha chomoza  si wajibu kwake kuilipa.

3- Pindi akifanya tendo moja wapo kati ya matendo yafunguzayo  kwamakusudi  kutokana na kupewa habari ya kuwa bado ni usiku kisha ikabainika kinyume chake.

4- Ikiwa atapewa habari ya kuwa alfajiri imechomoza na akafanya jambo lifunguzalo  kwa madai kuwa alie toa habari alikuwa akifanya mzaha  katika habari alizo zitoa  kisha ikabainika  ya kuwa alfajiri ilikuwa imekwisha chomoza.

5-Ikiwa   atapewa habari na mtu anae  sikilizwa kauli yake kisheria  kama dalili ya kuwa jua lime zama na akala kisha ikabainika  kinyume chake, ama ikiwa alie toa habari ni mtu asie tegemewa  na kusikilizwa kauli yake ni wajibu kutoa kafara vile vile isipokuwa ikigundulika ya kuwa  kufungua huko kulikuwa baada ya kuzama jua.

6- Ikiwa mwenye  funga atakula kwa kuitakidi kuwa jua limezama  kisha ikibainika kinyume chake, hata kama hali hiyo itasababishwa na kuwepo mawingu angani kwa kauli ya ahwat.

HUKUMU ZA KADHAA ( KULIPA FUNGA)

Hauzingatiwi utaratibu  wala kufuatanisha katika ulipaji wa funga,  kwani inajuzu kutenganisha  katika funga hizo  kama ambavyo inajuzu kulipa funga zilizo pita  kwa mara ya pili kabla ya kulipa zilizo mpita kwa mara ya mwanzo.

Mas’ala: Kauli ya awlaa na ahwat ni kuwa mukallaf  atalipa funga zilizo mpita katika mwezi wa ramadhani  katika mwaka ulele hadi kufikia ramadhani ifuatayo, na asiicheleweshe katika mwaka huo, lau kama ataichelewesha  kwa makusudi itambidi kutoa kafara kwa kila siku kibaba kimoja kutokana na kauli ya ahwati ya wajibu, vilevile  ikiwa ataichelewesha  bila kukusudia pia,  ndio ikiwa kucheleshwa huko kulitatokana na kuendelea kwa ugonjwa  hadi ikafika ramadhani nyingine, na mukallaf hakuweza kuilipa katika mwaka wote huo  wajibu wa kulipa utaporomoka na itamlazimu kutoa kafara tu.

Mas’ala: Ikiwa ita ainishwa ya kuwa ni wajibu kulipa  katika siku ambazo haijuzu kufunga katika siku hizo  kabla ya kupinduka jua na baada yake, ama ikiwa wakati ni mpana  inajuzu kufungua kabla ya kupinduka jua  na haita juzu baada yake, na kati makundi hayo mawili  lau kama atafungua  baada ya kupinduka kwa jua  itamlazimu kutoa kafara  nayo ni kuwalisha masikini kumi kila mmoja atampatia kibaba kimoja cha chakula, ama ikiwa atashindwa kutoa chakula hicho  badala yake  atafunga siku tatu,  ama funga nyingine ya wajibu- isiyo kuwa kadhaa ya mtu- ikiwa inafahamika kuwa ni funga gani haita juzu kufungua  katika siku hiyo- bali imethibiti katika siku hiyo kutoa kafara kama ikiwa atafungua katika siku maalum kwa ajili ya nadhiri- na ikiwa wakati wake ni mpana  inajuzu  kufungulia katika siku hiyo kabla ya  adhuhuri na baada ya adhuhuri,  na awlaa ni kuwa asifungulie baada ya kupinduka kwa jua na hasa ikiwa wajibu wenyewe ni kumlipia  mtu mwingine funga  ya mwezi wa ramadhani  kwa kuchukua malipo au mengineyo.

Alie pitwa na funga za mwezi wa ramadhani kutokana na udhuru  au kwa sababu nyineyo na hakukusudia kuilipa pamoja na kuwa alikuwa na uwezo wa kufunga  hadi akafariki  kauli ya ahwat  ya wajibu ni kuwa  mwanae mkubwa wa kiume atamlipia kwa kuzingatia masharti mawili yaliyo tangulia kwenye mas’ala ya kadhaa za sala, na kauli ya ahwatul awlaa  ni kuwa atafanya hivyo kwa mama pia, na hukumu tuluyo itaja katika mas’ala ya kadhaa ya sala   hadi  kwenye  hukumu ya nne hadi katika kulipa sala  hukumu hiyo itatumika katika kulipa funga pia.

Mas’ala: Ikiwa mtu atapitwa na funga  ya mwezi wa ramadhani kwa sababu ya maradhi, hedhi, au nifasi na hakuweza kuzilipa  kwa mfano akafariki kabla ya kupona kutokana na maradhi yale au hedhi na nifasi hiyo au baada ya kupona na kabla ya kupita muda  ambao inafaa kulipa katika zama hizo hata lipiwa funga hiyo.