Miongoni mwa mambo makubwa kabisa ya wajibu katika dini ni kuamrisha mema na kukataza maovu, Mwenyezi Mungu alie takasika amesema:
ولتكن منكم أمة يدعون إلى الخير ويأمرون بالمعروف وينهون عن المنكر وأولئك هم المفلحون».
(Na wawepo katika nyinyi kundi lenye kulingania kheri, na kuamrisha mema na kukataza maovu, na hao ndio watakao faulu).
كيف بكم إذا فسدت نساؤكم، وفسق شبابكم، ولم تأمروا بالمعروف ولم تنهوا عن ا لمنكر فقيل له: ويكون ذلك يا رسول اللّه؟ قال (ص) : نعم. فقال: «كيف بكم إذا أمرتم بالمنكر، ونهيتم عن المعروف، فقيل له: يا رسول اللّه (ص) ويكون ذلك؟ فقال: نعم، وشر من ذلك كيف بكم إذا رأيتم المعروف منكراً والمنكر معروفاً؟».
Nyinyi mtakuwa katika hali gani pindi wanawake wenu watakapo haribika na kuwa mafisadi, na vijana wenu kuwa waovu, na hamkuamrisha mema wala kukataza maovu, akaulizwa Mtume (s.w.a) Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hayo yatakuwa (yatatokea)? Mtume (s.w.a) akasema: Ndio. Kisha akasema: Mtakuwa katika hali gani pindi mtakapo amrisha maovu na kukataza mema, akaulizwa Mtume (s.w.a): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hayo yatakuwa? Akasema: Ndio na mabaya zaidi ya hayo. Pia mtakuwa katika hali gani pindi mtakapo yaona mema kuwa ni maovu na maovu kuyaona mema?
Na zimepokelewa riwaya kutoka kwao (Rehma na amani ziwe juu yao) zikisema ya kuwa: Hakika kwa kuamrisha mema, faradhi na mambo ya wajibu kusimamishwa na kutekelezwa, na hupatikana matumaini ya kutojitokeza na kuwepo kwa madhehebu, na mapato huwa ya halali, na kuzuilika kwa dhuluma, na ardhi kujengeka na kuimarika kwa wema na Mwenye kudhulumiwa kurudishiwa haki yake kutoka kwa dhalimu, na watu wataendelea kuishi katika kheri maadamu wana amrisha mema na kukataza maovu (mabaya), na wakasaidizana juu ya mambo mema, ikiwa hawakufanya hivyo basi baraka zitatolewa kwao (watanyang'anywa baraka) na baadhi yao kutawalishwa juu ya wengine na hawata kuwa na msaidizi ardhini wala mbinguni.
MAS'ALA 1270: Ni wajibu kuamrisha mema yaliyo wajibu, na kukataza maovu (mabaya), na wajibu huu ni wajibu wa kifai, kwa maana kuwa ikiwa mtu mmoja wapo atajitokeza na kutekeleza wajibu huu basi wajibu huo unakuwa umeporomoka na kuanguka kwa watu wengi, isipokuwa yule mwingine akiwa na ihtimali yakuwa alie amrishwa hatatekeleza wala kukatazika kwa yale aliyo amrishwa na kukatazwa, na kwamba lau kama ataamrisha yeye hayo mema na kukataza maovu kuna ihtimali na matarajio ya kuathirika mwenye kuamrishwa na kukatazawa hayo mabaya, na kama hakujitokeza yeyote na kutekeleza jukumu hilo wote watapata dhambi na wote watastahili adhabu.
MAS'ALA 1271: Ikiwa mema hayo ni mambo ya sunna basi kuamrisha mema hayo litakuwa ni jambo la sunna, na mwenye kuamrisha mambo hayo atastahili kupata thawabu, na ikiwa hakuamrisha mambo hayo hatakuwa na Thawabu wala Adhabu.
Katika kuamrisha mema na kukataza mabaya hushurutishwa mambo yafuatayo:
1- Kuyafahamu mambo mema na mabaya hata kama ni kwa sura ya ujumla, kwa hivyo basi si wajibu kwa mtu asiye yajua mambo hayo kuamrisha mema na kukataza maovu.
2-Kuwe na ihtimali au matarajio ya kuwa mwenye kuamrishwa mema atafuata mema hayo na kukatazika mwenye kukatazwa maovu, ikiwa hakuwa na matarajio au ihtimali kama hiyo na akafahamu ya kuwa mfanyaji wa maovu hajali maamrisho na makatazo yake, na wala hatayajali mambo mawili hayo, haitakuwa ni wajibu kwake kufanya chochote.
3- Mfanyaji wa maovu awe ni mwenye kuendelea na kitendo cha kuacha kufanya mema, na awe ni mwenye kuendelea kufanya maovu, ama kukiwa na alama iashiariayo kuacha kwake kufanya maovu na kuto endelea kwake na kitendo chake cha kuto kufanya mema, bali haita kuwa ni wajibu kwa kuwa tu na ihtimali juu ya hayo, kwa mfano mwenye kuacha mambo ya wajibu, au mwenye kufanya mambo ya haram na haikufahamika ya kuwa ni mwenye kuendelea na kitendo chake cha kuacha kufanya mambo ya wajibu au kufanya mambo ya haram kwa mara ya pili, au haikufahamika ya kuwa ameachana na azma na dhamiri yake ya kufanya hivyo, au ni mwenye kujuta kwa kufanya kwake vile, haitakuwa ni wajibu kwake kufanya chochote, haya ni kuhusiana na mwenye kuacha kufanya mema, au alie fanya maovu nje.
Ama yule ambae anakusudia kuacha kufanya mema, au anaekusudia kufanya maovu ni wajibu kumuamrisha kufanya mema na kumkataza kufanya maovu, hata kama hatakusudia kufanya hivyo isipokuwa mara moja tu.
4- Mema na maovu yawe ni yenye kufahamika vema kwa mfanyaji na yawe ni munajjaz kwake (yaani yawe yamethibiti kwake kuwa ni maovu), ama akiwa ni mwenye udhuru katika kufanya kwake maovu au katika kuacha kwake kufanya mema, kwa kuitakidi kuwa aliyo yafanya ni halali (Mubaha) na si haram, au akawa na itikadi ya kuwa aliyo yaacha si ya wajibu, na akawa ni mwenye kukubaliwa udhuru wake katika hayo kutokana na kuto pambanua na kuyatambua maudhui (yaani alikuwa na ishtibahi katika maudhui), au akawa ni mwenye kukubaliwa udhuru wake katika hukumu kutokana na ijtihadi yake aliyo ifanya au kutokana na kufanya kwake taqliid, haitakuwa ni wajibu kufanya chochote. Ndio, huenda ikawa ni wajibu kumuelekeza na kumuongoza mtu asie jua maudhui katika sehemu ambazo imethibitika ya kuwa sheria imezitilia mkazo na umuhimu mkubwa sehemu kama hizo kufanya matendo hayo bali ni wajibu kwake kufanya ihtiyaati hata kama atakuwa ni mwenye kughafilika na kutenda matendo hayo hukubaliwa udhuru wake na kusamehewa, na haya au sehemu hii haiingii katika uamrishaji wa mema na ukatazaji wa maovu.
5- Mtu asidhurike kwa sababu ya kuamrisha mema na kukataza maovu, au heshima yake na mali yake visidhurike kwa sababu ya kuamrisha kwake mema na kukataza maovu, na si yeye tu bali hata waislaam wengine, ikiwa italazimika kupata madhara kwa kufanya kazi hiyo au mtu yeyote kati ya waislaam, haitakuwa ni wajibu kufanya chochote, na kauli ya dhahiri ni kuwa hakuna tofauti kati ya kufahamu ya kuwa kutatokea madhara au kuwa na dhanna (kudhania) kuwa yatatokea madhara hayo au kuwa na ihtimali, ihtimali ambayo hutiliwa maanani na watu wenye akili na ambayo hupelekea kuthibitika kuwepo kwa khofu (woga), haya ni pale atakapo kuwa hakuthibitisha wazi ya kuwa kuamrisha kwake mema na kukataza kwake maovu hakutoathiri. Ama ikiwa atathibitisha ya kuwa kutatoa athari, hapo hapana budi kuliangalia jambo litakalo kuwa na umuhimu zaidi, kwani pengine huenda ikawa wajibu kuamrisha mema na kukataza maovu pamoja na kufahamu ya kuwa kuna madhara yatakayo jitokeza kutokana na kufanya kwake kazi hiyo, seuze kuwa na dhanna ya kutokea kwa madhara hayo au kuwa na ihtimali ya kutokea kwake.
MAS'ALA 1272: Kuamrisha mema na kukataza maovu hakuhusiki na watu Fulani pekee na kuto husika na watu wengine, bali yanapo timia masharti yake inakuwa ni wajibu kwa mwanazuoni na wengineo, kwa muadilifu na fasiki (muovu), utawala na wananchi wa kawaida, matajiri na masikini, ikiwa mmoja wapo atasimama na kutekeleza jukumu hilo basi kwa wengine huporomoka wajibu huo, isipokuwa katika baadhi ya sehemu kama ilivyo tangulia, na ikiwa hakujitokeza yeyote na kutekeleza jukumu hilo wote kwa pamoja watapata dhambi, na watastahili kupata Adhabu.
Kuna hatua kadhaa katika kuamrisha mema na kukataza maovu nazo ni kama zifuatazo:
1- Kupinga na kukemea kwa ulimi na kutumia kauli kama vile kumpatia mawaidha, kumnasihi na kumtajia aliyo yaandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waasi (Adhabu iumizayo na adhabu ya moto), au kumtajia aliyo yaandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wenye kutii amri zake au wenye kumtii yeye kama vile thawabu nyingi watakazo zipata na kufaulu kuingia kwenye pepo zenye neema.
2- Kupinga na kukemea kwa moyo, kwa maana ya kwamba, kudhihirisha kuchukizwa na kukerwa na maovu au kuacha kutenda mema, ima kwa kudhihirisha kukerwa kwako na mfanya maasi au kujiepusha nae na kuto mjali au kumtenga au kuto zungumza nae na mfano wa hayo, kama vile kufanya matendo Fulani au kuacha matendo Fulani yathibitishayo kuchukizwa kwako na matendo ayafanyayo.
3- Kupinga na kukemea kwa kutumia mkono kama vile kupiga pigo lenye kuumiza limzuialo mfanya maasi kutenda maasi yake, na kila hatua moja kati ya hatua hizi ina hatua ya juu na chini zaidi, (kwa maana kuwa kuna hatua dhaifu na iliyo ngumu), na kauli iliyo mashuhuri ni kufuatanisha katika utekelezaji wa hatua hizi kwa maana kuwa kuanza na hatua ya kwanza kisha kufuatia ya pili kisha inayo fuatia pamoja na kutanguliza hatua ya pili kabla ya hatua ya kwanza, ikiwa kudhihirisha kukerwa na kuto ridhia matendo yale kimoyo kuna tosheleza kumzuwia kufanya maovu basi atakomea kwenye hatua hiyo, laa sivyo atakemea kwa kutumia ulimi, ikiwa haikutosheleza kutumia ulimi atakemea kwa mkono wake, lakini kauli iliyo dhahiri ni kutanguliza ukemeaji wa kutumia ulimi kabla ya kukemea kwa moyo, yaani kudhihirisha kukerwa na matendo yale kama ilivyo tangulia, na pengine huenda ikalazimika kujumuisha mambo mawili hayo. Ama hatua ya tatu hufuatia ikiwa hatua mbili za mwanzo hazikuathiri, bali kauli ya ihtiyat katika kifungu hiki na hatua zake zote ni kuwa italazimika kuomba ruhusa kwa Haakimush-sharii’i laa sivyo kuthibiti kwa matendo hayo kuwa ni katika kuamrisha mema na kukataza maovu kunas ishkali.
MAS’ALA 1273: Ikiwa hatua zilizo tajwa hazikutosheleza kumzuia mfanya maasi, kujuzu kuhamia kwenye hatua ya kujeruhi na kuuwa, kuna wajihi mbili: Bali kuna kauli za aina mbilina yenye nguvu zaidi kati ya kauli hizo ni kuto hamia kwenye hatua hizo.
Vile vile ikiwa italazimika kuvunja kiungo kimoja wapo cha mkono au mguu na vinginevyo, au kukitia kasoro kiungo Fulani kama kukifanya kipooze au kukipindisha na mfano wa hayo, hakika kauli yenye nguvu ni kuwa haijuzu hivyo, na ikiwa kupiga kutapelekea kutokea mambo kama hayo kwa bahati mbaya au kwa kukusudia- kauli yenye nguvu ni kuwa atakuwa na dhamana atakae fanya hivyo.
Na atahukumiwa amefanya kosa la jinai kwa kukusudia, ikiwa alifanya makusudi, na atahukumiwa kuwa amefanya kosa lisilo la kukusudia ikiwa ilitokea kwa bahati mbaya. Ndio, inajuzu kwa imam na Haakim shar'ii kufanya hivyo ikiwa maasi ya mtenda maasi yatasababisha uharibifu mkubwa zaidi na ambao madhara yake ni makubwa zaidi kuliko kumjeruhi au kumuua, na wakati huo hakuta kuwa na dhamana yoyote kwa mfanyaji au mtekelezaji wa amri hiyo.
MAS’ALA 1274: Husisitizwa zaidi na kutiliwa mkazo suala la kuamrisha mema na kukataza maovu kwa kila mtu au katika haki ya kila mukallaf kuhusiana na familia yake na watu wake, kwa hivyo itakuwa ni wajibu kwake ikiwa atawaona wanazembea na kutotilia umuhimu utekeleza wa mambo ya wajibu, kama kusali na sehemu zake na masharti yake kama akiona hawatekelezi kama ipasavyo, kwa kutosoma vema na kuto soma dhikiri za wajibu au hawatawadhi vizuri udhu ulio sahihi au hawavitwahirishi viwili wili vyao na mavazi yao kutokana na Najisi kama inavyo takiwa, hapo atawaamrisha mema kwa utaratibu na kupitia hatua zilizo tangulia hadi wayatekeleze sawa sawa na inavyo takiwa, hivyo hivyo katika mambo mengine ya wajibu.
Vilevile ikiwa atawaona wanazembea katika utendaji wa mambo ya haram kama kusengenya na kuteta na uchonganishi na kufanyiana uadui wao kwa wao, au kuwafanyia wenzi wao, na mengineyo kati ya mambo ya haram, hakika ni wajibu kwake kuwakataza na kuwakemea kufanya maovu hadi waachane na utendaji wa maasi na katika sehemu hii hutumika hatua ya tatu bila ya kuwepo haja ya kuomba ruhusa kwa Hakimushar'ii.
MAS’ALA1275: Ikiwa mtu atafanya maasi bila ya kutarajia au bila kukusudia na ikafahamiaka ya kuwa si mwenye azma ya kuendelea kufanya maasi hayo haita kuwa ni wajibu kumuamrisha mema na kumkataza maovu hata kama hakutubia, ndio, ikiwa hajui kuwa ni wajibu kutubia na kwamba tawba hufuta madhambi itawajibika kumuongoza na kumuelekeza.
Baadhi ya waheshimiwa (Mwenyezi Mungu autukuze utajo wao) wamesema: Hakika moja kati ya vielelezo vya kuamrisha mema na kukataza maovu na kilicho bora kabisa na cha hali ya juu na kilicho thabiti na kigumu zaidi hasa kuhusiana na uongozi wa dini ni kujipamba kwa vazi la mema, wajibu, sunna na avue vazi la maovu, haram na makruhu, na aipambe nafsi yake kwa maadili na tabia bora, na aiepushe nafsi yake na tabia mbaya na zilizo kemewa, kwani kuonekana mambo kama hayo kwake ni sababu tosha ya kuwafanya watu watende mambo mema na ni sababu ya kuwafanya kuacha maovu na kujiepusha nayo hasa ikiwa atayakamilisha hayo kwa mawaidha mazuri yenye kuvutia na yenye kutisha, kwani kila mahala kuna maneno yake maalum, na kila gonjwa lina dawa yake, na kuzitibia nafsi na akili ni kugumu zaidi kuliko kuvitibia viwiliwili kwa daraja kadhaa (hatua kadhaa) na ikiwa atafanya hivyo, wakati huo atakuwa ametekeleza moja wapo kati ya vielelezo vya juu kabisa vya kuamrisha mema na kukataza maovu.
Jambo la kwanza: Katika sehemu hii tutataja mambo mema.
Kati ya hayo ni haya yafuatayo:
1-Kushikamana na Mwenyezi Mungu mtukufu:
«ومن يعتصم باللّه فقد هدي إلى صراط مستقيم»
(Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu hakika ameongozwa kwenye njia aliyo nyooka) na Abu Abdillahi (a.s) amesema: (Mwenyezi Mungu alie takasika alimteremshia wahyi Nabi Daud na kusema: Hashikamani na mimi mja yeyote kati ya waja wangu, bila ya yeyote kati ya waja wangu kufahamu hilo katika nia yake, kisha mbingu na dunia na vyote vilivyomo kumfanyia vitimbi na hila isipokuwa humuwekea matokeo na nja ya kuepukana na vitimbi hivyo).
Kati ya hayo ni: Kumtegemea Mwenyezi Mungu alietakasika, mpole na rahim kwa waja wake na mwenye kufahamu maslahi yao na mwenye uwezo wa kutatua na kukidhi mahitaji yao. Na ikiwa hakumtegemea na kutawakali kwake alie tukuka basi atawakali kwa nani je atawakali juu ya nafsi yake? Je atawakali kwa mwinginewe pamoja na kushindwa kwake na kuto fahamu kwake? Mwenyezi Mungu amesema:
«ومن يتوكل على اللّه فهو حسبه»
(Na mwenye kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu basi yeye ndie mwenye kumtoshelezea mambo yake). Na Abi Abdillahi (a.s) amesema:
«الغنى والعز يجولان، فإذا ظفرا بموضع من التوكل أوطنا».
(Utajiri na izza (utukufu) ni vitu vinavyo zunguka kila mahala, pindi vinapo pata mahala ambapo kuna tawakkuli basi hupafanya kuwa makazi yake).
Kati ya mambo mema ni: Kuwa na dhanna nzuri na Mwenyezi Mungu mtukufu, Amirilmuuminiin (a.s) amesema katika mazungumzo yake:
«والذي لا إله إلا هو لا يحسن ظن عبد مؤمن باللّه إلا كان اللّه عند ظن عبده المؤمن، لأن اللّه كريم بيده الخير يستحي أن يكون عبده المؤمن قد أحسن به الظن، ثم يخلف ظنه ورجاءه، فأحسنوا باللّه الظن وارغبوا إليه».
(Nina apa kwa haki ya yule ambae hapana mola isipokuwa yeye hakuna mja yeyote mwenye kumfanyia Mwenyezi Mungu dhanna nzuri isipokuwa Mwenyezi Mungu huwa na mja wake katika dhanna ya mja wake muumini, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mkarimu mikononi mwake kuna kheri zote huona haya kuona mja wake muumini anakuwa na dhanna nzuri naye kisha yeye kwenda au kufanya kinyume na dhanna yake na matarajio yake, kwa hivyo kuweni na dhanna nzuri na Mwenyezi Mungu na pendeni kuwa na dhanna nzuri na mola wenu.
Kati ya hayo ni: Kuwa na subira wakati wa mitihani (kuwa mvumilivu), na kuwa mvumilivu katika mambo yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu alie takasika amesema:
«إنما يوفى الصابرون أجرهم بغير حساب»
(Hakika watu wenye subira (wavumilivu) watapewa hesabu ya matendo yao bila hesabu). Na Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema katika hadithi:
«فاصبر فإنّ في الصبر على ما تكره خيراً كثيراً، واعلم أن النصر مع الصبر، وأن الفرج مع الكرب، فإن مع العسر يسراً، إن مع العسر يسراً»،
(kuwa na subira kwani kusubiri na kuwa mvumilivu kwa yale ayachukiayo kuna kheri nyingi, na fahamu ya kuwa ushindi uko pamoja na wenye kusubiri (wavumilivu), na kwamba faraja hutokana na matatizo, hakika kila lililo zito linawepesi wake, hakika kila zito lina wepesi wake.
Na Amirul-muuminiin (a.s) amesema:Subira hainyimwi ushindi hata kama muda wa kusubiri utakuwa mrefu sana, na amesema (a.s) kuna aina mbili za subira: 1- Kuwa na subira wakati wa msiba na aina hii ya subira ni nzuri, na iliyo nzuri zaidi ya hiyo ni kusubiri (kuwa mvumilivu) juu ya yale aliyo yaharamisha Mwenyezi Mungu).
Kati ya mema hayo ni: Kumcha Mungu (kujilinda na maasi), Abu Jaafar (a.s) amesema:
«ما عبادة أفضل عند اللّه من عفة بطن وفرج»
(Hakuna ibada iliyo bora kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kulihifadhi tumbo na utupu kutokana na mambo ya haram).
Abu Abdillahi (a.s) amesema: Hakika si vinginevyo mfuasi (Shia) wa Jaafar (a.s) ni yule alie lihifadhi tumbo lake na utupu wake na jihadi yake kuwa kubwa na akafanya amali kwa ajili ya muumba wake, na akataraji thawabu zake na akaogopa adhabu yake, ukiwaona watu kama hao elewa kuwa hao ndio mashie (wafuasi) wa Jaafar (a.s).
Kati ya hayo ni: Upole, Mtume (s.w.a) wa Mwenyezi Mungu amesema:
«ما أعزّ اللّه بجهل قط، ولا أذل بحلم قط»
Mwenyezi Mungu hamtukuzi mja kwa ujinga kamwe, wala hajamdhalilisha kamwe mja alie mpole. Na Amiril-muuminiin (a.s) amesema:
«أول عوض الحليم من حلمه أن الناس أنصاره على الجاهل»،
Kitu cha kwanza apewacho mtu mpole kama mbadala kutokana na upole wake ni kuwa watu humnusuru kwa mtu mjinga). Na Imam Ridhaa (a.s) amesema:
«لا يكون الرجل عابداً حتى يكون حليماً».
(Mtu yeyote hawi ni mfanya ibada wa kweli mpaka awe mpole).
Kati ya mambo hayo ni: Unyenyekevu, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w):
«من تواضع للّه رفعه اللّه، ومن تكبر خفضه اللّه، ومن اقتصد في معيشته رزقه اللّه، ومن بذّر حرمه اللّه، ومن أكثر ذكر الموت أحبّه اللّه تعالى».
(Mwenye kufanya unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu humuinua daraja yake, na mwenye kutakabari Mwenyezi Mungu humshusha daraja yake, na mwenye kufanya iqtisadi (mipango mizuri katika matumizi yake) Mwenyezi Mungu humruzuku, na mwenye kufanya matumizi mabaya Mwenyezi Mungu humnyima, na mwenye kukumbuka sana mauti (kifo) Mwenyezi Mungu humpenda.
Kati ya hayo ni: Kuwafanyia watu uadilifu (Insafu), hata kama ni kwako mwenyewe, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w):
«سيد الأعمال إنصاف الناس من نفسك، ومواساة الأخ في اللّه تعالى على كل حال».
(Bwana wa amali zote ni kuwa na Insafu katika nafsi yako, na kumlewaza nduguyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kila hali).
Kati ya hayo ni: Ni mtu kujishughulisha na aibu zake na kuacha aibu za watu wengine. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w):
«طوبى لمن شغله خوف اللّه عز وجل عن خوف الناس، طوبى لمن شغله عيبه عن عيوب المؤمنين»
Ni uzuri ulioje wa mtu alieshughulishwa na kumuogopa Mwenyezi Mungu na kutojishughulisha na kuwaogopa watu, ni uzuri ulioje wa mtu ajishughulishae na aibu zake na kuto jishughulisha na aibu za waumini).
«إن أسرع الخير ثواباً البر، وإن أسرع الشر عقاباً البغي، وكفى بالمرء عيباً أن يبصر من الناس ما يعمى عنه من نفسه، وأن يعير الناس بما لا يستطيع تركه، وأن يؤذي جليسه بما لا يعنيه».
Hakika kheri ya haraka zaidi kumpatia mtu thawabu na malipo mazuri ni matendo mema, na sharri ya haraka zaidi kumpatia mtu adhabu ni matendo maovu, na yatosha kuwa ni aibu kwa mtu kuyaona ni ya aibu wayafanyayo watu wengine na kuyafumbia macho yale ayafanyayo yeye mwenyewe, na kuwaaibisha watu wengine kwa mambo asiyo weza kuyaacha, na kumuudhi rafiki yake au mtu anae kaa nae kwa mambo yasiyo muhusu).
Kati ya hayo ni: Kuirekebisha nafsi pindi inapo mili kwenye mambo ya sharri, amesema Amiril-muuminiin (a.s):
«من أصلح سريرته أصلح اللّه تعالى علانيته، ومن عمل لدينه كفاه اللّه دنياه، ومن أحسن فيما بينه وبين اللّه أصلح اللّه ما بينه وبين الناس».
(Mwenye kujirekebisha ndani ya nafsi yake Mwenyezi Mungu humrekebishia dhahiri yake, na mwenye kufanya matendo kwa ajili ya dini yake Mwenyezi Mungu humtoshelezea mambo ya dunia yake, na mwenye kuyafanya mema yaliyoko kati yake na Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu huyasuluhisha na kuyarekebisha yaliyoko kati yake na watu wengine).
Kati ya hayo ni: Kujiepusha na dunia (kuwa na zuhdi) (yaani kuto ipenda dunia) Abu Abdillahi (a.s) amesema:
«من زهد في الدنيا أثبت اللّه الحكمة في قلبه، وأطلق بها لسانه، وبصره عيوب الدنيا داءها ودواءها، وأخرجه منها سالماً إلى دار السلام»،
Mwenye kuitupa mkono dunia Mwenyezi Mungu huithibitisha hekima moyoni mwake, na kuufungua ulimi wake na kumuonyesha aibu za dunia, magonjwa yake na tiba (dawa) yake), na kumtoa kwenye dunia hiyo akiwa salama na kumuweka kwenye nyumba ya amani (Darus salaam), mtu mmoja akasema kumwambia Aba Abdillah (a.s) (Hakika mimi sikutani na wewe isipokuwa baada ya miaka kadhaa basi niusie jambo ili niweze kushikamana nalo na kulishikilia? Imam akasema (a.s): Ninakuusia kumcha Mwenyezi Mungu, na kujikinga na maovu na kufanya jihadi, na jihadhari usiyatilie tamaa (usiyatamani) ya mtu alie na uwezo kuliko wewe, na yatosha kaul ya Mwenyezi Mungu alipo sema kumwambia Mtume wake (s.a.w):
«ولا تمدن عينيك إلى ما متعنا به أزواجاً منهم زهرة الحياة الدنيا»
(Wala usivikodolee macho yako tulivyowastareheshea watu wengi miongoni mwao, ni mapambo ya maisha ya dunia. Na pia Mwenyezi Mungu amesema:
«فلا تعجبك أموالهم ولا أولادهم»
(Na wala usishangazwe na kuvutiwa na mali yao wala watoto wao).
Ikiwa utayaogopa hayo basi yakumbuke maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) kwani chakula chake kilikuwa kikitokana na ngano, na halwa yake ni tende, na kuni zake ni makuti ya mnazi zinapo patikana, na ukipatwa na msiba (balaa) katika nafsi yako au mali yako au mwanao, basi ukumbuke msiba wako au msiba uliokupata kwa kuondokewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) kwani hakuna kiumbe yeyote alie patwa na msiba mfano wa msiba wa Mtume (s.a.w).
BAADHIYA MAMBO MABAYA NA MAOVU:
Kati ya maovu hayo ni: Kuchukia, (kughadhabika). Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema: (Ghadhabu inaharibu imani kama vile siki inavyo haribu Asali), na Abu Abdillahi (a.s) amesema: (Ghadhabu ni Ufunguo wa kila jambo la shari (baya). Na Abu Jaafar amesema (a.s): Hakika mtu huchukia (hughadhabika) na kutoridhia kamwe hadi anaingia motoni, kwa hivyo basi mtu yeyote anapo chukia na kuwaghadhabikia watu wake (familia yake) hali ya kuwa
Amesimama basi akae chini haraka (wakati ule ule), kwani ataondokewa na uchafu wa shetani, na mtu yeyote akichukia na kumghadhabikia ndugu yake basi amsogelee na kumgusa, kwani udugu unapo gusana ghadhabu hutulia na kupoa).
Kati ya hayo ni: Husuda, (kuhusudu) Abi Abdillah (a.s) amesema: Hakika husuda inakula Imani kama vile moto ulavyo kuni. Na Mtume (s.a.w) siku moja alisema kuwambia mashwaba wake: (Kwa hakika Mme ambukizwa na kuemnewa na ugonjwa wa kaumu na nyumati zilizo tangulia kabla yenu, nao ni husuda si wenye kunyonyoa nyele, lakini ni wenye kuiondosha na kuiteketeza dini, na mwenye kutaka kuokoka na kusalimika na ugonjwa huo basi na auzuie mkono wake, na kuutia huzuni ulimi wake, na asiwe ni mwenye kumuaibisha na kumkusudia ndugu yake muumini kwa sharri).
Kati ya hayo ni: Dhulma (kudhulumu), Abu Abdillahi (a.s) amesema: Mwenye kufanya dhuluma ya aina yoyote itachukuliwa dhulma yake hio katika nafsi yake au katika mali yake au katika kizazi chake). Na pia amesema (a.s) Hajafanikiwa jambo la kheri mwenye kufaulu kufanya dhulma (mwenye kudhulumu) ama ukweli ni kuwa mwenye kudhulumiwa huchukua katika dini ya mwenye kudhulumu zaidi ya ayachukuayo dhalimu kwenye mali ya mdhulumiwa).
Kati ya hayo ni: Watu kujikinga na shari zake, Mtume (s.a.w) amesema: (Watu waovu kabisa kwa Mwenyezi Mungu siku ya kiama ni wale ambao hukirimiwa kwa kuogopwa na kujikinga na shari zao). Na Abu Abdillahi (a.s) amesema: (Mtu ambae watu huuogopa ulimi wake basi huyo ni mtu wa motoni). Na pia amesema (a.s): Hakika kiumbe mwenye kuchukiwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni mja ambae watu huuogopa ulimi wake).
Wal-hamdu lillahi awwalan wa akhira, wahuwa hasbuna waniimal-wakiil.